Watu 55 wafariki katika ajali ya basi Kenya wakielekea Kisumu, Magufuli atuma rambirambi

Gari baada ya ajaliHaki miliki ya pichaAFP

Watu 55 wamefariki dunia nchini Kenya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupata ajali kwenye barabara kuu ya Nairobi-Kisumu.

Walioshuhudia wanasema kuwa ajali hiyo ilitokea leo mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.

Ajali hiyo mbaya ilitokea katika eneo la Fort Ternan Kaunti ya Kericho.

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ni miongoni mwa waliotuma salamu za rambirambi kwa Wakenya.

Ameandika: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya basi iliyotokea Kericho nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 50. Nakupa pole Mhe. Rais Uhuru Kenyatta, familia za marehemu na Wakenya wote. Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema na majeruhi wapone haraka.”

Rais Kenyatta ametuma rambirambi kwa jamaa za waliofariki au kuumia na kuwataka madereva kuwa waangalifu zaidi barabarani.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi Kaunti ya Kericho, James Mogera, basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 67, lilipoteza mwelekeo barabarani baada ya dereva kushindwa kulimudu, kisha kugonga vizuizi vilivyokuwa kando ya barabara na kubingiria mita 20 kwenye bonde.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Nation, miongoni waliofariki ni watoto wanane wa chini ya umri wa miaka mitano.

Awali idadi ya waliofarini ilikuwa 40 lakini polisi walielezae hofu yao juu ya vifo kuongezeka kutokana na hali ya baadhi ya majeruhi kuwa mbaya.

“Bahati mbaya sana tumepoteza watu 51,” Mkuu wa Polisi Kenya Joseph Boinnet ameiambia redio ya Capital FM.

Paa la gari hiyo lilifumuka baada ya kupinduka na kubiringia mara kadhaa.Haki miliki ya pichaAFP
Image captionPaa la gari hiyo lilifumuka baada ya kupinduka na kubiringia mara kadhaa.

Mmoja wa walioshuhudia anasema alisikia honi, ikifuatwa na mlio mkubwa wa breki, kisha akawasikia abiria wakipiga kelele.

Baadhi ya majeruhi wanatibiwa katika Zahanati ya Fort Ternan, huku wengine wakikimbizwa hadi kwenye Hospitali ya Kaunti mjini Muhoroni kwa matibabu.

Taarifa zaidi zinasema miili ya baadhi ya watu waliofariki ingali imekwama ndani ya mabaki ya basi hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *