Sababu ya vurugu kukumba magari ya mwendo kasi Tanzania

Mabasi ya mwendo wa kasi TZ
Image captionMabasi ya mwendo wa kasi TZ

Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka maarufu kama mabasi ya Mwendokasi umekuwa tegemeo kuu kwa wasafiri Dar es Salaam lakini kwa siku mbili, huduma hiyo imekumbwa na vurugu.

Tatizo hilo lilizidi leo ambapo mabasi yaliadimika sana na yaliyopatikana abiria walilazimika kung’ang’ania nafasi ndani.

Baadhi walitumia madirisha badala la milango, mradi tu wajipate ndani ya mabasi hayo.

Je, chanzo ni nini?

Mkuu wa mawasiliano wa kampuni ya Usafiri Dar es Salaam Rapid Transit (UDA-RT), ililopewa wajibu wa kuendesha huduma hiyo, ametoa taarifa inayoashiria kuwa mgomo wa madereva ndicho chanzo kikuu cha kuvurugika kwa usafiri.

Madereva walivyoshikilia mateka mabasi

Taarifa ya Bw Deus Bugaywa iliyotolewa leo inaeleza kuwa kwa kawaida shughuli ya kutoa mabasi kutoka kwenye karakata kwenda kuhudumu barabarani hufanyika kwendo wa saa kumi kasorobo alfajiri.

Huduma hutakiwa kuanza saa kuni unusu na hivyo huwa kuna muda wa kutosha kwa madereva kuandaa magari tayari kwa safari.

Karakana ya mabasi hayo inapatikana eneo la Jangwani.

Leo, shughuli ilianza lakini badala ya kuendelea kama kawaida dereva mmoja alichukua basi na kuliegesha eneo la ndani la lango kuu la kutokea upande wa mbele na hivyo akawa ameziba njia. Mabasi mengine hayangeweza kutoka.

Basi lililotumiwa kuziba lango lilikuwa na urefu wa mita 18.

Kulikuwa na ndereva mwingine ambaye aliziba lango la nyuma kwa kutumia basi kama hilo.

Kutoroka na funguo

Baada ya kuziba milango mikuu, madereva hao wanadaiwa kuondoa funguo kutoka kwenye eneo la kuwashia magari na kukimbia hadi nje ya uzio na kutokomea.

Hii iliifanya vigumu kuyaondoa mabasi yaliyokuwa yameziba milango hiyo na ilihitaji mafundi kuitwa.

Rais Magufuli ndani ya basi la Mwendo Kasi katika baada ya kufungua rasmi Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam 25 Januari, 2017Haki miliki ya pichaIKULU, TANZANIA
Image captionRais Magufuli ndani ya basi la Mwendo Kasi katika baada ya kufungua rasmi Awamu ya Kwanza ya Miundombinu na Utoaji Huduma ya Mabasi yaendayo Haraka katika jiji la Dar es Salaam 25 Januari, 2017

Taarifa ya Bw Bugaywa inasema walinzi walijaribu kuwafuata madereva hao wawili bila mafanikio.

Baadaye mafundi walifanikiwa kuyaondoa magari, lakini madhara yalikuwa tayari yametokea.

“Kazi hiyo ilifanikiwa lakini tayari ratiba ilikuwa imevurugika sana na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria.

“Tunaamini kitendo hicho kilifanywa makusudi kwa lengo la kuhujumu mradi na ndio maana uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vya dola unafanyika ili kuwabaini tote waliohusika na njama hizo.

Tunaomba radhi abiria wetu kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na kuchelewa kuanza huduma.”

Mishahara ya madereva

Bw Bugaywa amekiri kamba kumekuwa na mzozo kuhusu mishahara ya madereva na wahudumu wa mabasi hayo.

Amesema mishahara ya wafanyakazi ya Septemba ilianza kulipwa Jumatatu, siku ambayo pia ilikumbwa na vurugu.

“Hatuoni saabu ya kuunganisha tukio hili na mishahara,” amesema Bw Bugaywa.

Watanzania wamekuwa wakilalamika kwenye mitandao ya kijamii:

Athanas Pius ameandika: “Huu sio usafiri wa mwendokasi tena, sasa hivi ni mwendokusubiri 😭😭. Watu mnajazana kituoni zaidi ya masaa mawili na hakuna gari. ”

“Hili shirika la UDART limeoza, Hiyo kimara leo, kituo kimejaa mpk sio poa,” aliandika kwenye ujumbe mwingine.

Brighton Pepee naye akaandika: “Ukitaka kutambua umuhimu wa mpinzani awepo katika jambo lolote ili asiwe na kiburi fatilia mwenendo mzima wa mabasi ya mwendo kasi wanajua hawana mbadala huwezi kwenda mjini bila wao wanafanya kazi wanavyotaka utaenda wapi ukapate usafiri wa kukufikisha uendako xhubamiiit.”

Suphian Juma naye akasema: “Wananchi walitegemea ‘pepo’ katika usafiri wa Mwendokasi Dar ila sasa ni kukanyagana, kuibiana, kugusana maungo ya mwili, kukosa hewa, kuumizana na kuambukizana magonjwa….

“Serikali rudisheni daladala kwani naona kutokuwa na mshindani, Mwendokasi wanabweteka, hawajali uhai wa watu.”

Jwise 017 naye: “Kwa hali hii sisi wa mkoani tuliokua na ndoto ya kuja Dar kupanda mwendokasi hatuji tena.”

UDART walikuwa Jumatatu wameandika ujumbe kuomba radhi kutokana na usumbufu uliotokea siku hiyo, lakini wakaonekana kulaumu idadi ya mabasi.

Waliahidi: “Tunaendelea kuwaomba uvumilivu kama tulivyotoa taarifa kuwa mtoa huduma wa pili atapatikana baada ya kumaliza taratibu za manunuzi ya serikali kati ya Mwezi Januari-Machi mwaka 2019.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *