Mauaji ya Watoto: Waganga wa jadi wajitenga na matukio ya mauaji ya watoto Njombe, Tanzania

Waganga wa jadi
Image captionBaadhi ya Waganga wa tiba za jadi wilayani Njombe wakijadiliana jambo baada ya mkututano na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani

Waganga wa tiba za jadi wilayani Njombe nchini Tanzania wamejitenga na tuhuma kuwa wanachochea mauaji ya watoto wilayani humo.

Kwa mujibu wa serikali, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji ya watoto sita wilayani humo yamechochewa na imani za kishirikina.

Watoto hao, wakiwemo watatu wa familia moja wenye umri chini ya miaka 10 wamepatikana wakiwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha huku baadhi ya viungo vyao kama macho, meno na sehemu za siri vikinyofolewa.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola Jumatano aliliambia Bunge kuwa imani za kishirikina zimechochea matukio hayo na tayari serikali ina majina ya wahusika wote.

Hata hivyo, katika kikao chao na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni wilayani Njombe waganga wa jadi wamesema wao si chanzo cha tatizo na kuitaka serikali ifanye uchunguzi zaidi

Kiongozi wa waganga wa tiba za jadi Antony Mwandulami amedai kuwa watu wamekuwa wakilipiziana visasi kwa mauaji na kusingiziwa waganga wa jadi.

“Kuna mambo mengi nyuma ya haya mauaji. Wapo ambao wanalipiziana visasi na hawaonekani lakini waganga wanalaumiwa kwa kusemwa kuwa wamepiga ramli chonganishi,” amesema Mwandulami.

Hofu yatanda

Image captionMsafara wa mazishi ya watoto watatu wa familia moja waliokumbwa na mkasa huo.

Mwandishi wa BBC Swahili Leonard Mubali anaripoti kutoka Njombe kuwa hofu imetanda wilayani hapo kutokana na matukio hayo ya mauaji.

Wazazi wameongeza uangalifu kwa watoto zao, na kuna ambao wanaacha shughuli zao na kusindikiza watoto shule.

Akizungumzia hofu hiyo waziri Masauni amesema: “Nachotaka kuwahakikishia wananchi ni kuwa macho, masikio, roho na moyo wa serikali umehamia Njombe. Waamini kuwa serikali jambo hili tumelichulia uzito mkubwa… ni jukumu letu kuwalinda wananchi ambao ndio wameiweka serikali hii madarakani. Lazima tuhakikishe kuna ulinzi, na hilo lipo ndani ya uwezo wetu na wala hatuna msalie mtume.”

Akizungumzia kikao na waganga wa jadi Masauni amesema lengo lilikuwa ni kuunganisha nguvu na kupata taarifa zaidi kutoka kwao hususan kuwataja wale ambao wanachochea uovu.

Image captionWaziri Masauni (katikati) akiogoza moja ya vikao wilayani Njombe kujadili mikasa hiyo ya mauaji ya watoto.

Mtu mmoja, kutoka kwenye familia ya watoto watatu waliouawa yumo mikononi mwa polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Juzi Jumanne kuliibuka suitafahau baada ya wananchi wa Njombe kutaka kumpiga bwana mmoja ambaye wanadai alitaka kumteka mwanafunzi wa shule ya msingi.

Polisi iliwalazimu kutumia mabomu ya machozi ili kuutawanya umati huo wa watu wenye hasira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *