Job Ndugai: Je, Spika wa Bunge Tanzania ana mamlaka ya kumuamuru CAG kwenda kuhojiwa na kamati ya Bunge?

Job Ndugai
Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amemwamuru Prof Musa Assad kufika bungeni

Kauli ya Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ya kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Musa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge imepokelewa kwa hisia kali nchini Tanzania.

Katika mkutano na wanahabari jana Jumatatu Spika Ndugai ametishia iwapo Prof Assad hatatii wito huo siku ya Januari 21 kwa hiari yake, atapelekwa kwa nguvu na kufungwa pingu.

Hivi karibuni, Profesa Assad alifanya mahojiano na radio ya Umoja wa Mataifa Idhaa ya Kiswahili nchini Marekani na kusema Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

“…Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa,” Profesa Assad ameiambia radio ya UN.

Assad ameongeza kuwa: “Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, maelezo ya Assad yameonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili wa Bunge na inampasa ajieleze mbele ya kamati.

Spika ana mamlaka?

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa, wanaharakati, wachambuzi na watumiaji wa mitandao ya kijamii wameipinga kauli hiyo ya Spika Ndugai wakidai kuwa hana ya mamlaka ya kumwita.

Hoja yao wanaijenga kwa msingi wa ibara ya 143 (6) ya Katiba ya Tanzania ambayo inampa kinga CAG ya kufuata maagizo ya mtu yeyote isipokuwa uchunguzi wa mahakama.

Ibara hiyo kwa ukamilifu inasomeka: “Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.”

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Prof Musa Assad akiwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu mstaafu Ludovick S. L. UtouhHaki miliki ya pichaNAO.GO.TZ
Image captionMdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Prof Musa Assad akiwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu mstaafu Ludovick S. L. Utouh

Ofisi ya CAG imejizoelea sifa miaka ya karibuni nchini Tanzania hususani katika uongozi wa raisi aliyepita Jakaya Kikwete kwa kuibua kasha za ubadhirifu kwenye ripoti ambazo zililiwezesha bunge kuibana serikali ipasavyo.

Lakini kumekuwa na hisia ambazo Prof Assad amezithibitisha kuwa kuwa kwa sasa bunge halitumii ipasavyo ripoti za ofisi hiyo kuibana serikali.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amedai kuhojiwa CAG na kamati ya bunge itakuwa ni udhalilishaji.

Kauli hiyo ya Zitto ingawa iliungwa mkono na wengi wapo ambao waliitilia mashaka na kuhoji kile alichokisema CAG. Mmoja wa walioonesha mashaka ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Tanzania ambaye alikuwa mshirika mkubwa wa kisiasa wa muda mrefu wa Zitto, Profesa Kitila Mkumbo.

Alipotakiwa kutoa tathmini ya ufanisi wa bunge lililopo sasa na yale yaliyopita Profesa Mkumbo alisema tathmini ni mawazo binafsi.

Wapo ambao wanaona Spika Ndugai amelichukulia jambo hilo kuwa binafsi, na hata kama angelikuwa na mamlaka ya kumuita CAG ni Bunge ndilo mabalo lingemuelekeza kufanya hivyo.

Maoni hayo yametolewa pamoja na wengine na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Fatma Karume na wakili Jebra Kambole.

Naye wakili maarufu wa kujitegemea na mwanachama wa chama tawala CCM Alberto Msando kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ameiita kauli ya Spika Ndugai kuwa ni “kichekesho kibaya sana.”

Awali alipohojiwa na mwandishi wa BBC Abubakar Famau juu ya ukomo wa mamlaka yake kwenye suala hilo na wachambuavyo baadhi ya watu Spika Ndugai alijibu: “Sasa wamshauri (CAG Prof Assad) kuwa asije (mbele ya kamati ya Bunge) halafu ndio wataona nini kitatokea.”

Kumwondoa kazini CAG

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, CAG huondoka madarakani baada ya kufikisha umri wa kustaafu ama kujiuzulu wadhfa wake.

Ibara 144 ya katiba pia inasema CAG aweza kuondolewa katika madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote) au kwa sababu ya tabia mbaya, au kwa kuvunja masharti ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, kuna utaratibu maalumu wa kumwondoa ambapo ibara ya 144 (3) inabainisha kuwa iwapo rais ataona kwamba suala la kumwondoa kazini CAG lahitaji kuchunguzwa, basi ataunda kamati atateua Tume Maalum ambayo itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiopungua wawili.

Mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa Tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni Majaji au watu waliopata kuwa Majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.

Iwapo Tume itamshauri rais kwamba huyo CAG aondolewe kazini kwa sababu ya kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya, basi Rais atamwondoa kazini.

Wakati wa uchunguzi, rais anaweza kumsimamisha kazi CAG. Lakini uamuzi huo utabatilika ikiwa Tume itamshauri Rais kwamba huyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu asiondolewe kazini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *