Ukataji miti hovyo umeleta changamoto TANAPA.

Ukataji miti hovyo na uchomaji  wa mkaa ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili shirika la hifadhi  za taifa nchini TANAPA katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini.

Mkurugenzi wa  utumishi  na utawala  wa TANAPA  Witness Shoo amesema hayo wakati wa hafla ya   Kufunga Mafunzo ya ujasiriamali na mradi  wa ufugaji nyuki  kwa vijana wa ulinzi shirikishi yaliyofanyika katika kijijiji cha Manda  Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Amesema kuwa shirika hilo limetoa mafunzo hayo ya ujasiriamali kwa vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuwajengea uwezo wa kipato na kujiendeleza wenyewe ikiwa ni pamoja na kuwapatia mizinga 120 na vifaa vya kulina asali katika awamu ya kwanza kwa lengo la  kuunga mkono kaulimbiu ya serikali ya viwanda  ya Rais John Magufuli.

Pamoja na  changamoto hizo Meneja wa ujirani Mwema wa TANAPA  Ahmed  Mbugi   amesema kuwa  awamu hiyo ya kwanza  ya mafunzo  iliyohusisha vijiji vya  Chinuguli  Ilandali  na Manda imesaidia kuleta ufanisi katika maeneo ya hifadhi kwa kupunguza vitendo vya ujangili baada ya vijana waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivyo kushirikishwa kwenye mradi wa nyuki.

Awali akisoma Risala kwa mgeni rasmi mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo ya ulinzi shirikishi Emmanuel Stefano amesema kuwa mafunzo hayo yamesaidia kuimarisha ushirikiano baina ya hifadhi na jamii na kupunguza ujangili kwa asilimia kubwa.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa  mkoa wa Dodoma,mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga amewapongeza TANAPA Kwa mpango huo wa ulinzi shirikishi ili kulinda hifadhi za Taifa huku akikemea vitendo vinavyoashiria Rushwa kwa viongozi wa vijiji ambavyo vinapelekea kuendelea kwa uharibifu wa mazingira na uvamizi wa hifadhi za Taifa.

Pia mkuu wa wilaya amevipongeza vijiji  vyote vitatu kwa kutoa maeneo ya kusaidia vijana kwenye mradi wa ulinzi shirikishi kwa kuwa zimetolewa zaidi ya shilingi milioni 44 na TANAPA  kuendesha mafunzo na  kununua vifaa huku kampuni ya Ruaha Farm ikichukua jukumu la kununua asali kwa asilimia mia moja.

#Sibukamedia

Comments

comments