Timu ya wanawake Kenya walazwa 3-1 na Ghana nchini Cameroon

hara

Utata ulikumba mechi ya ufunguzi ya timu ya taifa ya Kenya, Harambee Starlets iliposhindwa mabao 3-1 na Ghana katika mechi ya mchuano wa kuwania kombe la taifa bingwa Afrika kwa upande wa wanawake (Awcon) kufuatia maamuzi tata mjini Limbe usiku wa Jumapili.

Esse Mbeyu Akida alikuwa ameiweka Kenya kifua mbele katika kipindi cha kwanza kabla ya utepetevu wa safu ya ulinzi ya Kenya kusababisha Samira Souleyman kusawazishia Ghana mapema baada ya mapumziko.

Hata hivyo refarii Jeanne Ekoumou raia wa Cameroon aliibua hisia kali miongoni mwa timu ya taifa ya Kenya ya wanawake aliponyoosha mkono wake akiashiria mkwaju wa penalti ilhali tukio la utovu wa nidhamu lilikuwa limetokea nje ya eneo la lango.

Hata hivyo mashabiki waliokuwa uwanjani walighadhabishwa mno na uamuzi huo wa refa Ekoumou baada ya picha za runinga zilizoonyeshwa uwanjani kuonesha wazi kuwa mchezaji wa Kenya aliyeunawa mpira alikuwa nje kabisa ya eneo la lango.

Lakini kama kilio cha kuku ambacho hakimpati mwewe, Ghana hawakuchelea, walifuma mkwaju kimiani na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele wakiongoza mabao 2-1 kunako dakika ya 71 ya kipindi cha pili.

Mfungaji wa tobwe hilo akiwa ni nahodha Elizabeth Addo.

Dakika moja baadaye refarii huyo alichomeka msumari wa moto kwenye kidonda cha Kenya alipopuuzilia mbali ombi la Kenya la penalti mshambulizi Esse Mbeyu Akida alipoangushwa mbele ya lango na walinzi wa Ghana.

Bi Ekoumou akaonesha wazi ishara ya kuwa ni penalty kwa upande wa Kenya.Lakini baada ya dakika chache za majadiliano na msaidizi wake alibadilisha kauli hiyo na kuwapa the Black Queens wa Ghana mkwaju wa adhabu. Wakenya waliteta na kubisha lakini wapi.

Bi Ekoumou alisimama kidete na kupuliza kipenga mpira uendelee. Kwanzia hapo ilikuwa bayana kuwa Wakenya walikuwa washapoteza ari ya kucheza na haikuwa ajabu kombora la Portia Boakye lilipotikisa wavu wa Kenya kipa wao Samantha Akinyi akiwa ameduwaa.

Bao hilo la dakika ya 91 ya mechi hiyo ilikuwa msumari wa mwisho katika jeneza la wakenya waliosalia wananongoneza jinsi maamuzi yalivyoponza ndoto yao ya kusunga mbele katika kidumbwedumbwe hicho chao cha kwanza kuwahi kushiriki.

Hayo yalijiri huku mabingwa watetezi Nigeria wakitangaza wazi ari yao kwa kuwanyeshea Mali mabao 6-0 katika mechi ya ufunguzi ya kundi Ba. Mshambulizi wa , Arsenal Asisat Oshoala alifungua kivuno hicho cha mabao kwa kufunga mabao 4 na kuwaongoza Super Falcons kuthibitisha udedea wao.

Kufuatia ushindi huo Super Falcons wanahitaji kuilaza Black Queens ya Ghana katika mechi ijao ilikujihakikishia nafasi katika raundi ya pili ya nusu fainali ya mchuano huo.

Kenya itarejea uwanjani Jumatano tarehe 23 huko huko Limbe Cameroon kumaliza udhia dhidi ya Mali.

Hapo kesho Cameroon watachuana dhidi ya Afrika Kusini huku Zimbabwe ikikabiliana na Misri katika uwanja wa Omnisports Ahmadou Ahidjo, ulioko Yaoundé Cameroon.

#BBC

Comments

comments

Random Posts