Tanzania: Uchaguzi mdogo wa Buyungu wakosolewa na Marekani

 

Marekani imeeleza kutoridhishwa na uchaguzi mdogo uliofanyika mnamo tarehe 12 mwezi Agosti nchini Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam inasema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia na makosa mengi.

Ubalozi huo pia ulieleza wasiwasi kuhusu vitisho vilivyotolewa na maafisa wa polisi dhidi ya wanachama wa upinzani, kukamatwa kiholela kwa wanasiasa, na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

”Masuala hayo yanahujumu haki ambayo katiba ya Tanzania inawapatia raia wake na kuhatarisha amani na utulivu nchini na katika kanda yote,” ilisema taarifa hiyo.

Msemaji wa serikali, akijibu taarifa hiyo ya ubalozi aliandika kwenye Twitter: “Kuna taarifa inasambaa kuhusu kinachodaiwa ni taarifa ya ubalozi mmoja kuhusu masuala ya ndani ya nchi. Tunajiridhisha. Tutatoa tamko punde.”

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baadaye ilitoa taarifa ikiutaka ubalozi wa Marekani uthibitishe taarifa zake kuhusu uchaguzi mdogo wa Buyungu na kata 36.

Tume hiyo ilishangaa ni wapi ubalozi huo ilitoa taarifa hizo kwa kuwa uchaguzi huo haukuwa na waangalizi wa kimataifa.

Mnamo tarehe 12 mwezi Agosti Tanzania ilifanya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Buyungu, jimbo la Kigoma na wadi 36 nchini humo.

Uchaguzi wa Buyungu ulifanyika ili kujaza pengo lililoachwa baada ya kifo cha mbunge wa awali Kasuku Bilago aliyekuwa wa chama cha upinzani Chadema.

Bilago alifariki dunia mwezi Mei.

Mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM Christopher Chiza, ambaye ni waziri wa zamani alitangazwa mshindi eneo bunge hilo na tume ya uchaguzi nchini humo NEC.

Kulingana na NEC, bwana Chiza alijipatia kura 24,578 na kumshinda mgombea wa Chadema Elia Fredrick Michael kwa jumla ya kura 7,668. Fredrick alijipatia kura 16,910.

Katika wadi zote 36 ambapo uchaguzi huo ulifanyika madiwani wa chama cha CCM walitangazwa washindi.

Viti hivyo vilikuwa wazi baada ya baadhi ya madiwani kujiuzulu kutoka upinzani na kujiunga na chama tawala CCM. Katika baadhi ya maeneo madiwani walifariki na wengine wakavuliwa uanachama wa vyama vyao kwa sababu zisizojulikana.

Nini kinachowafanya wanasiasa kuhama vyama?

Miaka ya nyuma mwanasiasa akihama katika chama chake ilikuwa ni jambo zito sana, lakini kwasasa mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vimegubikwa na taarifa za wanasiasa wanaohama vyama vyao mara kwa mara.

Chama tawala cha CCM ndio kimbilio la wapinzani.

Kwani kwa takribani mwaka sasa viongozi wa ngazi mbali mbali katika vyama vya upinzani wamehamia CCM.

Kwa zaidi ya wiki moja mfululizo wanasiasa ikiwemo wabunge na madiwani kutoka chama cha CUF na Chadema wametangaza kujiengua katika vyama vyao ikiwemo kujiuzulu nafasi zao za uongozi.

Naibu meya wa manispaa ya ilala, na diwani wa vingunguti Omari kumbilamoto amejiuzulu nafasi ya udiwani na umeya lakini pia amejivua uanachama wa CUF.

Mbunge wa jimbo la Monduli kwa Tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Julius Kalanga Laizer amejiuzulu na kujiunga na CCM kwa kile alichoeleza kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Kabla ya kalanga kujiuzulu alikuwa ni mwanasiasa wa upinzani, Mwita Waitara alitangaza kujiengua katika chama kikuu cha upinzani cha chadema na kujiunga na Chama tawala, CCM.

Waitara aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Ukonga lililopo Dar es salaam alikishutumu chama cha Chadema, kuwa hakina demokrasia pia kutokuwa na maelewano na mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe.

Ikumbukwe kuwa wabunge hawa wote yaani Waitara na Kalanga waliwahi kuitumikia CCM, ambapo Waitara aliitumikia CCM mwaka 1998 mpaka mwaka 2008 wakati Kalanga aliwahi kuwa diwani kupitia CCM.

Sheria inasemaje

Kwa mujibu wa sheria wanasiasa hawa, wabunge, madiwani na Meya wamejiengua katika nyadhifa zao zote walizopata katika uchaguzi mwaka 2015, hivyo majimbo yao yako wazi.

Hata hivyo baada ya kujiengua baadhi yao wamepata neema ya kuteuliwa na rais katika baadhi ya nafasi za uongozi. Wiki iliyopita Rais Magufuli alimteua David Kafulila kuwa katibu tawala wa mkoa wa Songwe.

Awali Kafulila alikuwa mbunge wa chama cha upinzani NCCR-Mageuzi.

Pia alimteua Moses Machali kuwa mkuu wa wilaya ya Nanyumbu. Kabla ya uteuzi huo Machali aliwahi kuwa mbunge wa Kasulu mjini kupitia NCCR-Mageuuzi ambapo baadaye alihamia ACT-Wazalendo kisha kwenda CCM.

Mwanasiasa mwingine aliyepata fursa hiyo ya kuteuliwa na Rais ni Patrobas Katambi ambaye amekuwa mkuu wa wilaya ya Dodoma, Kabla ya hapo Katambi alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la vijana la Chadema.

Comments

comments