Tanzania: Mzee Kimweri Dafa apewa zawadi ya kusherehekea miaka 100 ndani ya ndege ya Dreamliner

Mzee wa miaka 100 amesherehekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa kwa kusafiri na ndege kwa mara ya kwanza, kama zawadi aliyopewa na mtoto wake.

Akizungumza na mwandishi wa BBC Halima Nyanza ndani ya ndege, huku jicho akilitupa dirishani mara kwa mara kupata mandhari nzuri ya anga, kwa sauti ya utulivu bila ya woga, mzee Kimweri Dafa Kivo amesema anasikia furaha kutokana na kuwa ni mara yake ya kwanza.

Isitoshe, amekuwa miongoni mwa Watanzania wa mwanzo mwanzo walioabiri ndege mpya iliyonunuliwa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) na kupokelewa mwezi uliopita.

”Mwanangu namshukuru sana kwa sababu aameweza kunipandisha kwenye ndege, nimefurahi sana..” amesisitiza mzee Kimweri.Akizungumzia zawadi aliyompa baba yake mtoto wa mzee Kimweri, Imam Dafa anasema ilimchukua muda kufikiria juu ya nini cha kumpa baba yake.

”Nilikuwa nafikiria kwa kumshukuru Mungu na kumpa baba zawadi kwa kufikia umri huo nifanye nini, nilifikiria sana, basi nikaona nimpe baba zawadi ya kupanda ndege kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 100…” alisema Imam.

Comments

comments