Serikali yajibu upya swali lililomponza Kitwanga

Dodoma. Kitendo cha Charles Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kujibu swali akiwa amelewa kimesababisha jibu lake kuwa batili na jana, Serikali ilitoa upya bungeni majibu kutokana na maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kitwanga, ambaye anatuhumiwa kuhusika kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa mkataba wa ufungaji mashine za kielektroniki za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi, alivuliwa uwaziri Ijumaa iliyopita baada ya kutinga bungeni akiwa amelewa na kujibu maswali kwa namna ambayo ilielezewa na muulizaji kuwa “ya pozi”.

Akijibu swali hilo, Kitwanga alijikita kusoma karatasi aliyokuwa nayo, akisitasita na kuweka vituo sehemu kadhaa huku akinyanyua kichwa kwa nadra.

“Mheshimiwa mwenyekiti, kama yalivyowahi kujibiwa maswali kadhaa ndani ya Bunge lako tukufu kuhusu askari kuboreshewa makazi, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na polisi kuishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi (anazungumza huku akitabasamu). Namuona rafiki yangu hapa anashusha kichwa, ananyanyua,” alisema.

“Mheshimiwa mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea na mpango wake wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba na kwenye baadhi ya Magereza na kujenga nyumba na vilevile kuendelea kuona mahitaji ya nyumba na hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221, hivyo kuwepo upungufu wa nyumba 10,279 ambao unalazimisha baadhi ya askari kuishi nje ya kambi za magereza.

“Hata hivyo, kasi ya utekelezaji umekuwa ni mdogo kutokana na ufinyu wa bajeti.”

Alipoulizwa kuwa Serikali itaendelea kujenga nyumba hadi lini wakati sasa ni miaka 54 ya uhuru, Kitwanga alianza kujibu kwa kuuliza swali: “Mheshimiwa mwenyekiti, huyu ni rafiki yangu. Ananiuliza wapewe miaka mingapi? Na yeye ana miaka mingapi?”

Jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusufu Masauni alijibu swali hilo namba 211 la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Devota Minja ambalo lilikuwa na tofauti kubwa kulinganisha na lililotolewa na Kitwanga Ijumaa asubuhi.

Kati swali hilo ambalo awali lilikuwa namba 205, Minja alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuboresha makazi ya polisi na magereza wanaoishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ikilinganishwa na kazi zao kwa jamii.

Kama ilivyokuwa wiki iliyopita wakati swali hilo lilipoulizwa na kwa niaba yake na Mbunge wa Mlimba (Chadema), Suzan Kiwanga, jana liliulizwa na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.

Tofauti kati ya majibu ya Kitwanga na Masauni ilijitokeza katika takwimu ya nyumba za Magereza, lakini kwa upande wa nyumba za polisi majibu yalikuwa sawa, isipokuwa tu naibu waziri alitoa takwimu za kila mkoa tofauti na mwenzake.

Masauni alisema Jeshi la Magereza limesaini mkataba na kampuni ya Poly Technologies ya China kujenga nyumba 9,500 kwenye vituo vyote vya magereza nchini.

Alisema Makao Makuu ya Magereza zitajengwa nyumba 472, Arusha (377), Dodoma (356) Dar es Salaam (952), Kagera (364), Kigoma (272), Kilimanjaro (390) na Lindi watajenga nyumba 233.

Mikoa mingine ni Manyara (206), Mara (378), Mbeya (622), Iringa (336), Morogoro (669), Mtwara (215), Mwanza (398), Pwani (384), Rukwa (358), Ruvuma (320), Shinyanga (337), Singida (299), Tabora (408), Tanga (382), KMKGM Dar (219), Chuo cha Ukonga (115), Chuo cha Kiwira (183), Chuo cha Ruanda (62), Chuo cha KPF (27) Bohari Kuu (82) na Bwawani nyumba 84.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi majibu yalikuwa ni yale yaliyotolewa na Kitwanga kuwa Serikali inakusudia kujenga nyumba 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwamo mikopo nafuu na yenye riba nafuu na miradi shirikishi kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali.

Comments

comments