SERIKALI imeombwa kuwasaidia wamiliki wa shule binafsi Mkoani Dodoma.

DODOMA

SERIKALI imeombwa kuwasaidia wamiliki wa shule binafsi Mkoani Dodoma ili waweze kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kuboresha shule zao ziweze kuchukua wanafunzi wengi hasa katika kipindi hiki ambacho serikali imehamia mkoani hapa.

Ombi hilo limetolewa na mkurugenzi wa shule ya msingi El Shaddai iliyopo mjini hapa Juliana Assey wakati wa mahafali ya nne ya darasa la saba yaliyofanyika shuleni hapo ambapo pia ameiomba Serikali kuwaingiza katika mgao wa kupata vitabu kama inavyofanya katika shule za serikali ili kuonyesha mchango wao katika sekta ya elimu unathaminiwa na serikali.

Akizungumza katika mahafali hayo Mkurugenzi wa Usajili wa shule Khadija Mcheka amesema serikali haibagui wanafunzi kwa kuwa wote ni wa kitanzania na kueleza namna anavyoweza kuwezesha kutatuliwa kwa changamoto utolewaji wa vitabu katika shule zisizo za serikali

Akisoma risala mmoja wa wahitimu hao Aliyah Kamando amesema pamoja na changamoto zinazowakabili shuleni hapo ikiwemo ukosefu wa maktaba,nyumba za walimu na maabara ya kompyuta wanaahidi kufanya vizuri kutokana na juhudi zao wenyewe.

Shule ya El shaddai ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi watatu ambapo kwa sasa ina wanafunzi 430 lengo likiwa ni kusaidia Serikali katika utowaji wa Elimu bora na kuongeza wasomi watakaowezaesha kupeleka Taifa mbele.

  • Mwandishi : Barnaba Kisengi.
  • #SIBUKAMEDIA

Comments

comments

Random Posts