Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 01 Agosti, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Masahisa Sato Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Sato amesema Japan itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania na ameomba kuharakishwa kwa mchakato wa utiaji saini mkataba wa ushirikiano katika kulinda uwekezaji kati ya Tanzania na Japan (Bilateral Investment Protection Agreement – BIPA) ili kuchochea kasi ya uwekezaji.

Mhe. Sato pia ameahidi kufuatilia miradi yote inayofadhiliwa na Japan hapa nchini na ambayo utekelezaji wake unasuasua ili kutatua vikwazo na kutekeleza miradi hiyo.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Sato kwa kutembelea Tanzania na amemuomba afikishe salamu na shukrani zake za dhati kwa Waziri Mkuu wa Japan Mhe. Shinzo Abe kwa ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Japan, uliowezesha kutekelezwa kwa miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja, umeme, maji na afya.

Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Sato kufikisha mwaliko wake kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan wakiwemo wenye viwanda vya magari, kuja nchini Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali na amemhakikishia kuwa Serikali itawapa ushirikiano wowote watakaouhitaji.

“Mwambie Waziri Mkuu Shinzo Abe kuwa kwa niaba ya Watanzania namshukuru sana na namuomba ushirikiano huu mzuri uendelee, waambie wafanyabiashara wa kampuni za magari waje hata kesho, tutahakikisha wanapata mazingira mazuri ya kuwekeza” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Susan Kolimba na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaharu Yoshida.

 

Comments

comments