Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Akitoa wito, Huku akipokea Madawati 80 Kutoka kwa wakala wa Misitu Tanzania

magu-1

Wito umetolewa kwa wakala wa misitu Tanzania(TFS) kuisaidia wilaya ya Kinondoni Mbao kwa ajili ya milango,madirisha na kuezeka paa katika shule za msingi ili kuunganisha nguvu za wadau wanaochangia maendeleo ya elimu nchini.

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Ally Hapi ametoa wito huo leo jijini Dar-es-Salaam wakati akipokea madawati themanini yaliyotolewa na wakala wa huduma za misitu Tanzania na kuongeza kuwa upo umuhimu mkubwa kwa wakala huo kusaidia wilaya yake ili kumaliza changamoto ya madarasa.

Hapi ameongeza kuwa baada ya changamoto ya madawati kutatuliwa imejitokeza changamoto ya vyumba vya madarasa ambapo mpaka sasa wilaya yake ina upungufu wa jumla ya vyumba 1068.

Mapema akizungumza katika makabidhiano hayo Maneja wa wakala wa huduma za misitu wilaya ya Kinondoni Bwana Alexander Mboya amemweleza mkuu wa wilaya kuwa wametoa msaada huo ikiwa ni mwendelezo wa maagizo yaliyotolewa bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii Pofesa Jumanne Maghembe ya kuwataka wakala kutengeneza madawati yasiyopungua elfu ishirini kwa kipindi cha mwaka huu.

Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Londa Bi Elgiver Kimaro ameushukuru wakala huo kwa msaada wa madawati hayo huku akiahidi kuyatunza na kuyalinda.

Madawati hayo yatagawiwa katika shule ya msingi Londa na Kigogo kwa uwiano sawa.

#SIBUKA MEDIA

#Imeandaliwa na Stanley Burushi

 

 

Comments

comments