Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS)

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dr Leonard Maboko ametembelea mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kufanya tathimini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za UKIMWI zinavyotekelezwa katika mikoa hiyo.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dr Mboko alisema kuwa kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa matokeo ya UKIMWI ya mwaka 2016/17 unaonesha maambukizi kwa mkoa wa Lindi yapo kwa asilimia 0.3 wakati kiwango cha kitaifa ni asilimia 4.7 kwa Tanzania bara.
Dr Maboko aliongeza kuwa hali hii haimaanishi kuwa kiwango cha maambikizi hakiwezi kuongezeka kwani ni wazi kabisa kuwa kuna fursa za kiuchumi ambazo zinaongezeka na kuongeza mwingiliano wa watu. Alishauri kuwa kinachotakiwa ni kuongeza jitihada katika kutoa Elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU pamoja na elimu ya mabadiliko ya Tabia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe Godfrey Zambi alisema kuwa Mkoa wa Lindi bado unaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwani uwezekano wa kuongezeka kwa kiwango cha maambukizi haupingiki.
Akizungumzia fursa katika Mkoa wa Lindi
alisema kuwa kwa sasa wawekezaji wanaanza kujitokeza hasa katika sekta ya madini japo bado wapo katika hatua za awali za uwekezaji, ongezeko la viwanda na shughuli nyingine za uvuvi pia zinaendelea katika Mkoa huo.
Aliongeza kuwa elimu ya mabadiliko ya tabia inaendelea kutolewa kwa kushirikiana na viongozi wa dini pia vijana rika na vikundi vya WAVIU vinatumika katika kutoa elimu.

Akizungumzia maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu Pima,Jitambue,Ishi alisema katika Mkoa wa Lindi unaendelea kufanya maandalizi ya Kimkoa na baada ya hapo kila mkuu wa Wilaya atapanga namna sahihi atavyozindua katika Wilaya yake. Pamoja na hayo shughuli za upimaji
zinaendelea katika kila shughuli zenye mjumuiko akitolea mfano nane nane.

Naye kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Lindi Bwana Emmanuel Lwero alisema kuwa Halmashauri ya Lindi inaendelea na utoaji wa Elimu ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU ambapo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameweza kudhibiti baadhi ya tabia hatarishi hasa kupunguza athari za mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zinapelekea kuongeza maambukizi ya VVU .ametaja mila hizo kuwa ni pamoja na kubadilisha utaratibu wa kucheza ngoma za usiku nakuchezwa mchana tena katika kumbi maalum zilizotengwa na Serikali.

Alisema kuwa wameweza kugundua baadhi ya madanguro ambapo kwa kushirikiana na Polisi wamefanikiwa kuyafunga.
Kuna baadhi ya mila kama za kuchezwa watoto wamezitafutia njia nzuri ambayo zinafanyika kwa kufata taratibu za serikali hili ni kwa kushirikiana na jeshi la Polisi.
Aidha Mkurugenzi wa halimashauri ya Ruagwa alizungumzia jitihada za wawekezaji wa madini aina ya Graphite (Bunyu) kuwa inaongezeka siku hadi siku hivyo ni muhimu kuweka njia sahihi za namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU kwa kuwa hicho ni kiashiria cha ongezeko la mwingiliano watu katika mkoa wa Lindi.
Bwana Andrea aliongeza kuwa kwa sasa halmashauri inajenga uwanja mkubwa wa mpira wa miguu ambao wanatarajia utaleta vijana wengi wakati wa mechi lakini pia mashabiki wa timu husika ,hivyo ni viashiria vingine ambavyo vitawaongezea wingi wa mwingiliano na kuiomba TACAIDS kuwaongezea nguvu katika jitihada za mapambano ya mapya ya VVU

Comments

comments