Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dr Leonard Maboko ameishauri

Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dr Leonard Maboko ameishauri Halmashauri ya Manispaa ya Songea  kushirikiana na wadau katika utekeleza  shughuli za kudhibiti maambukizi ya VVU .
Akizungumza na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bwana Joel Mbewe  alisema kuwa katika kutekeleza shughuli za UKIMWI ni muhimu kukaa na wadau ili kuona namna nzuri  ya kuzitekeleza. Alieleza kuwa kwa sasa fedha za wafadhili za udhibiti UKIMWI zinapungua siku hadi siku wakati maambukizi ya VVU bado yapo hivyo mkae na wadau kuona namna bora ya kushirikiana nao katika mapambano haya.
Kwa mujibu wa taarifa ya viashiria vya UKIMWI ya mwaka 2016/17 Ruvuma inamaambukizi ya VVU asilimia 5.6 ambayo ni zaidi ya kiwango cha Taifa cha asilimia 4.7.
Kwa maana hiyo Mkoa wa Ruvuma bado unahitaji jitihada za ziada ili kukabiliana na maambukizi hayo ikiwa ni pamoja na kubainisha maeneo yenye viashiria vya maambukizi ya VVU afua zifanyike katika maeneo hayo ambayo huenda ndio vikawa chanzo cha kuongeza maambukizi.
Kaimu katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bwana Joel alibainisha maeneo yenye viashiria vya maambukizi ya VVU kuwa ni pamoja na maeneo ya machimbo ya dhahabu,vito vya thamani, makaa ya mawe na kuwa hayo ndio maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu.
Akizungumzia upande wa mila na desturi alisema kuwa kwa sasa mila zilizopitwa na wakati zimepungua  kutokana na elimu iliyokuwa inatolewa mara kwa mara kwa wananchi.
Naye Matibu wa Kudhibiti UKIMWI wa Manispaa ya Songea Bi Zare Makaburi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI katika Halimashauri ya Manispaa ya Songea kwa mwaka 2017/18 kiwango cha maambukizi ya VVU  kwa Manispaa ya Songea katika kipindi cha mwaka 2017 ni 3.1 wakati waliopima walikuwa 88255 kati yao wanawake ni 48185 na wanaume 40070. Waliogundulika kuwa na maambukizi ya VVU walikuwa ni 2780 kati yao wanawake walikuwa 1729 na wanaume 1051. Aliongeza kuwa Hamashauri  ina vituo 26 vilivyosajiliwa vinavyotoa huduma ya mayunzo na matibabu (CTC) na jumla ya wagonjwa ni 25619 kati yao 12349 tayari wameanzishiwa dawa za ARV.
Aliongeza kuwa Halmashauri inaendelea  kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya  virusi vya UKIMWI kwa jamii kupitia klabu za vijana na watu wanaoishi na VVU ,kutoa mafunzo mahali pa kazi,kutoa shuhuda katika mikutano ya jamii,kuwahimiza wateja wote waliopo kwenye dawa za kufubaza VVU kujua wingi wa VVU kwenye damu zao; na kutoa elimu kupitia sinema pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya kuhusu kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU.
Aidha maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu Pima,Jitambue ,Ishi yanaendelea kwa kushirikiana na wadau na yanatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Agosti.
Aidha Dr Maboko alikutana na baadhi ya wawakilishi wa kamati  za kudhibiti  UKIMWI katika ngazi za  Kata ,Vijiji  na Mtaa  na kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii katika utoaji wa elimu kwa umma ili kupunguza maambikizi mapya  ya VVU.
Aliongeza kuwa endapo kamati hizo zitafanya kazi vizuri katika ngazi husika shughuli ya uraghibishi na malengo ya kufikia sifuri tatu yatakuwa rahisi zaidi na alihidi kutoa zawadi kwa kamati itakayokuwa bunifu na kufanya vizuri zaidi katika kutekeleza majukumu yake.
Aidha aliwasisitizia kuhakikisha wanakaa vikao vyote kulingana na mwongozo wa uundaji wa kamati za kudhibiti UKIMWI.
Nao wawakilishi wa kamati hizo walishukuru kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS na kuahidi kufanya vizuri kwani kwa kuwatembelea na kuongea nao imewatia hamasa ya kuwa wabunifu na kujiwekea vipaumbele katika kudhibiti maambikizi mapya ya VVU katika maeneo yao na hasa kutoa elimu ya kujinga.
 Dr Leonard Maboko alitembelea Mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma kwa lengo la kutathimini utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI kwenye Mkoa na Manispaa husika, kusisitizia kampeni ya Furaha yangu inayohusu upimaji wa VVU hasa kwa wanaume,upatikanaji kutoka vyanzo vya ndani kwa ajili ya utekelezaji endelevu wa afua za UKIMWI pamoja na upatikanaji wa takwimu sahihi za VVU na UKIMWI.

Comments

comments