Meya wa Dar amtumbua meneja wa kituo cha mabasi Ubungo

Baraza la madiwani Kinondoni limewasimamisha kazi vigogo wawili wa manispaa

Dar es Salaam. Wakati Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita akimsimamisha kazi Meneja wa kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT), Juma Iddi, Baraza la Madiwani Manispaa ya Kinondoni, nalo limewasimamisha kazi vigogo wawili wa manispaa hiyo kwa tuhuma za kusababisha hasara ya mabilioni ya shilingi.

Meya Mwita alichukua uamuzi huo jana asubuhi alipotembelea kituo hicho na kukumbana na uchafu uliokithiri, ubovu wa miundombinu, kasoro za mikataba na malalamiko ya wafanyabiashara wenye vibanda vilivyoezekwa kwa miti kutozwa kodi ya kati ya Sh30,000 hadi Sh60,000 kwa siku.

Kutokana na kasoro hizo, Mwita ambaye pia alitembelea dampo la Pugu na miradi mingine miwili ya jiji hilo, alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Sarah Yohana kutafuta mtu mwingine kukaimu nafasi ya Iddi.

Waliosimamishwa kazi na Baraza la Madiwani ni Mwanasheria wa Manispaa, Burton Mahenge na Mkuu wa Idara ya Uwekezaji, Einhard Chidaga kwa tuhuma za kushindwa kusimamia miradi saba ya manispaa.

Kati ya miradi hiyo upo wa Oysterbay Villa na Magomeni kota ambayo imefanyiwa tathmini na manispaa hiyo na kubaini upotevu wa mapato wa zaidi ya Sh6 bilioni.

Uamuzi huo una baraka zote za baraza hilo lililoketi juzi kwa saa tisa na kujadili mapendekezo ya kamati ya fedha kuhusu miradi hiyo.

Meya Mwita alifika Ubungo saa 5.30 asubuhi na kwenda moja kwa moja katika ofisi za kituo hicho kupewa maelezo. Hata hivyo, Meya huyo aliyekuwa ameambatana na madiwani kadhaa, hakutaka kuzungumza chochote na kuamua kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ya kituo alikokuwa akielekezwa na wafanyabiashara badala ya meneja na timu yake. “Nasitisha mkataba wa Kampuni ya Usafi ya Moto Investment na naagiza atafutwe mkandarasi mwingine, pia, kituo hiki kiendelee kutumika na baraza la madiwani litajadili na kutengua uamuzi wa kujenga kituo cha mabasi yaendayo kasi hapa, maana hakuna mbadala wa kituo kingine cha mabasi ya mikoani,” alisema Mwita.

Pia, alitembelea Dampo la Pugu ambalo bajeti yake kwa mwaka ni takribani Sh1 bilioni na kuagiza baraza la madiwani kuandaa utaratibu wa kuwa na madampo mengine maeneo ya Kigamboni, Kinondoni na Mkuranga ili kuokoa fedha.

Msafara wa meya huyo ulitembelea pia eneo la jiji hilo lenye eka sita lililopo Tabata Relini lililokodishwa kwa Kampuni ya Mwananchi Engenering inayolipa kodi ya Sh8 milioni. Jambo hilo lilimfanya kumuagiza mwanasheria wa jiji hilo, Jumanne Mtinangi kupitia upya mkataba huo ulioanza Agosti, mwaka jana.

Walivyosimamishwa Mwanasheria na Mkuu wa Idara Kinondoni

Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema madiwani wote bila kujali itakadi za vyama vyao waliazimia watendaji hao wasimamishwe kazi ili wapishe uchunguzi dhidi yao. Meya huyo aliitaja miradi mingine ambayo imepata hasara kuwa ni Coco Beach, Kituo cha Mabasi Makumbusho, Kiwanja cha Tole Drive kilichopo mkabala na Bwaro la Polisi Masaki.

Mingine ni kiwanja cha wazi kilichopo pembezoni mwa Ubalozi wa Marekani na kiwanja cha Hill Road cha Masaki ambacho mwekezaji aliingia mkataba na manispaa kwa ujenzi wa nyumba za kupangisha.

Comments

comments