Maalim Seif aibua mapya kuhusu kuhojiwa na polisi

Dar/Zanzibar. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi kusema limemwita katibu mkuu wa CUF ijumaa kwa ajili ya kumhoji kuhusu masuala ambayo hayakuwekwa wazi, wanasiasa nchini wamekuja juu wakisema hatua hiyo inaashiria ukandamizaji wa kisiasa, huku chama hicho kikisema kinasubiri tukio hilo ili kitoe msimamo.

Wakati wanasiasa wengi waliozungumza na Mwananchi wakipinga kitendo hicho kwa maelezo kuwa hakitasaidia kutafuta suluhu ya kisiasa Zanzibar, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa ameshauri wanasiasa kuiga utulivu wa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa licha ya kufanyiwa vitimbi.

Juzi, Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Hamdani Makame alisema, Maalim Seif Sharif Hamad ameitwa kuhojiwa huku Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi akisema kuna mambo mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa mwanasiasa huyo ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Lakini wanasiasa wanaona kitendo hicho hakifai.

“Hawa watu wameingia katika njia ya ukandamizaji,” alisema Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki.

“Wameiba kura wakati wa uchaguzi, sasa wanatumia mabavu kuwanyamazisha wote wanaodai haki.”

Msemaji huyo mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alisema Serikali ya CCM inapaswa kujifunza kutokana na makosa na akasisitiza kuwa kumkamata mwanasiasa na kumpeleka Mahakamani si suluhisho, bali ni kuongeza uhasama na ugomvi.

“Maalim Seif aliwahi kuwekwa kizuizini kwa amri ya  Mwalimu Nyerere (Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza) mwaka 1987 hadi 1991, lakini hiyo haikusaidia chochote. Maalim aliwahi kufunguliwa kesi ya uhaini lakini haikusaidia chochote,” alisema Lissu.

“Yaani huo uamuzi wa polisi kumhoji Maalim unaonyesha kuwa hawa watu hawajifunzi kutokana na historia ya nchi yetu.”

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alikosoa njia ambayo polisi wametumia.

Alisema badala ya kumuita kituo cha polisi, walitakiwa kuomba kukutana naye na kumfuata popote alipo na kuomba maelezo yake.

Alisema kitendo cha kumwita polisi na hali ya sasa ya Zanzibar ni kuchochea uhasama kati ya wananchi na Serikali.

Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alimshauri Rais John Magufuli, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, awatake polisi kusitisha mpango huo.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya alisema: “Tunaisubiri siku ya Ijumaa kwa hamu. Tutajua hatua ya kuchukua kama chama baada ya kuona hatua ambazo Maalim atachukuliwa.”

Kambaya alitaja makada wa CUF ambao alidai wamekamatwa na kuhojiwa na polisi kuwa ni Nassor Ahmed Mazrui, Mansoor Yussuf Himid na mwanamkakati wa Maalim Seif katika chaguzi zilizopita, Mohamed Sultan Mugheiry, maarufu kwa jina la Eddy Riyami.

Ismail Jusa Ladhu alisema sababu kubwa ni Uchaguzi Mkuu pamoja na ule uliofutwa, kauli ambayo iliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho-Bara, Magdalena Sakaya.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, Hamad Masoud Hamad alisema hatua hiyo ni njia mbadala ya kuwanyamazisha Wazanzibari ambao alidai kuwa wengi waliamua kumpa ridhaa Maalim Seif kuiongoza Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu ambao matokeo yake yalifutwa.

Alisema katibu huyo mkuu wa CUF ni kiongozi aliyekubalika kwenye nyoyo za Wazanzibari wengi, hivyo hatua ya kujenga hofu na mazingira ya kumdhalilisha hayatawarudisha nyuma.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Salim Abdalla Bimani alisema huu si wakati tena wa siasa za kutishana kwa kuitiana polisi kwa kuwa Wazanzibari wameshakuwa wanaelewa kila hatua na njia bora za kudai haki.

Mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Zanzibar, Habibu Ismail Rashid alisema: “Nahisi hii ni njia ya kutaka kumdhalilisha Maalim Seif ili atoke mioyoni kwa watu, lakini nawaambia hilo wasahau. Maalim Seif anapendwa bwana!”

Viongozi wa upinzani, hasa kutoka CUF wamekuwa wakihojiwa na Jeshi la Polisi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa marudio uliofanyika Machi 20.

Uchaguzi huo ulirudiwa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais. Alifuta matokeo hayo wakati ZEC ikiwa imeshatangaza matokeo ya majimbo 31, huku mengine tisa yaliyosalia yakiwa yameshahakikiwa.

Alisema sababu za kufuta matokeo hayo ni kukiukwa kwa sheria na kanuni za uchaguzi, lakini CUF ilipinga ikisema alichukua uamuzi huo peke yake na kususia kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio.

Comments

comments