Lissu, Zitto, Bulaya, Lema, Mdee wengine wawili wasimamishwa

Dodoma. Wabunge saba wa upinzani wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa vipindi tofauti baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka kanuni na kusababisha vurugu bungeni.

Akitangaza azimio la adhabu hizo ambazo ziliungwa mkono na wabunge katika kipindi cha jioni bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alisema Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Tundu Lissu wa Singida Mashariki  wote wa Chadema wamesimamishwa kuhudhuria mkutano wa tatu wa Bunge unaoendelea kuanzia jana na vikao vyote vya mkutano wa nne kwa makosa ya kukiuka kanuni na kuonyesha dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika na kuhusika kwa kiasi kikubwa kuchochea vurugu Januari 27.

Alisema wabunge Halima Mdee (Kawe), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Pauline Gekul, wote wa Chadema na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini –ACT Wazalendo) wameadhibiwa kutoshiriki katika mkutano wa Bunge unaoendelea kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na dharau kubwa kwa mamlaka ya Spika na kusababisha kuvurugika kwa shughuli za Bunge.

Mbunge wa mwisho kuadhibiwa alikuwa John Heche (Tarime Vijijini – Chadema) ambaye amezuiwa kuhudhuria vikao 10 mfululizo vya mkutano wa tatu kuanzia jana kutokana na kosa moja

Hata hivyo, Mkuchika alisema mbunge amepata adhabu ndogo kulinganisha na wenzake kutokana na kutoa ushirikiano kwa kamati yake kwa kutii wito kwa kufika na kujibu maswali yote kama yalivyoulizwa na kuheshimu vikao vyote vya kamati na mwenyekiti aliyeviongoza.

Taarifa za kuadhibiwa kwa wabunge hao zilianza kuzungumzwa jana asubuhi baada ya Mkuchika kuwasilisha hati ya taarifa ya kamati yake kuhusu baadhi ya wabunge kufanya vurugu bungeni na kudharau mamlaka ya Spika Januari 27.

Mkuchika alisema upo umuhimu  mkubwa wa bunge kutunga kanuni za maadili ili kudhibiti nidhamu kwa wabunge kwa lengo la kuhakikisha kuwa Bunge na hadhi yake vinadumishwa.

Wazungumzia adhabu

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana kabla ya adhabu hizo kutangazwa baadhi ya wabunge hao walisema wamesikia kamati imeshauri wasimamishwe.

Mdee alisema amesikia kuwa atasimamishwa kutokana na suala hilo na kwamba kamati imeshauri wabunge wengine wapewe adhabu kali ya kutokuhudhuria mikutano miwili ya Bunge.

“Kamati inaruhusiwa kutoa adhabu ya kutokuhudhuria Bunge kwa siku 10 lakini inaweza kushauri Bunge liazimie ili watu wapewe adhabu zaidi. Hivyo tunasubiri ila tutaingia mtaani kuwashtaki kwa wananchi kwa kuwa wanataka kutufunga mdomo,” alisema Mdee.

Zitto alisema anajua ipo nafasi ya kukata rufaa lakini hatafanya hivyo kwa kuwa anajua kuwa hizo ni njama za kuwafunga mdomo.

Bulaya alisema hizo ni njama za kutaka wasihudhurie hotuba ya bajeti inayotarajiwa kusomwa wiki ijayo hivyo watawashtaki kwa wananchi kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kueleza ukweli.

Comments

comments