Kwanini visa vya shule kuteketezwa Kenya vinakithiri?

 

Zaidi ya shule 10 zimefungwa nchini Kenya kufuatia kinachotajwa kuwa ni utovu wa nidhamu na uharibifu wa mali.

Shule 7 kati ya 10 zilizofungwa zimeteketezwa moto inatuhumiwa na wanafunzi.

Mabweni katika shule hizo yaliteketezwa moto wakati wanafunzi walipokuwa darasani wakidurusu jioni.

Wizara ya elimu nchini inasema huenda ghasia hizo zinatokana na uoga walio nao wanafunzi wa mtihani.

Je kuna ukweli gani katika hili?

Dickson Bandika, mwanafunzi wa zamani katika shule ya upili ya Kenyatta Mwatate pwani ya Kenya anasema kwamba wanafunzi wanaona ghasia na maandamano ndio njia pekee ya kuwasilisha malalamiko yao bila ya kutambuliwa, kulengwa na kuonewa kwa malalamiko wanayoyawasilisha.

Ameeleza kwamba katika kuepuka aibu ya matokeo duni ya mitihani, wanafunzi huzusha ghasia katika kutaka kukwepa mitihani hiyo.

‘Watu wanaogopa kuonekana mumeshindwa na shule fulani’.

Tulikuwa hatuna shida na mitihani ya ndani ya shule, tatizo linazuka inapokuwa mitihani ya kieneo ambapo matokeo huziorodhesha shule kwa ubora wake. Hiyo aibu ndiyo watu waliokuwa wanaiogopa’. Amesema Dickson.

Wizara ya Elimu inasema nini?

Amina Mohammed waziri wa elimu Kenya anasema wanafunzi walizusha ghasia kupinga hatua kali zilizoidhinishwa hivi karibuni na wizara kuzuia udanganyifu katika mitihani.

Ameeleza kuwa katika shuel mbili, wanafunzi waliokuwa wanagoma walitaka mwalimu mkuu awaahidi kuwa atawasaidia kudanganya katika mtihani mkuu wa mwisho wa kufuzu kuingia vyuo vikuu.

‘Kwa zaidi ya miaka miwili wizara ya elimu imekaa ngumu sana na baadhi ya wanafunzi wa shule ya upili wana shinikizo kubwa sana la kutaka kupita mtihani, na sababu nyingine ni kesi za kawaida za utovu wa nidhamu tu’ amesema waziri wa elimu Kenya, Amina Mohammed.

Onyo kali la Polisi :

Polisi nchini Kenya imetoa onyo kwamba wanafunzi watakaopatikana na hatia katika ghasia zinazoshuhudiwa kwenye shule tofuati nchini watachukuliwa hatua za kisheria ambazo zitasalia kuwa rekodi ya uhalifu wa wanafunzi hao.

Kauli hiyo imeungwa mkono na wizara ya elimu nchini.

Kadhalika wanafunzi watachukuliwa hatua kuwazuia wanafunzi hao kuingia katika vyuo vikuu nchini au hata kupata ajira katika miaka ijayo.

Tayari wanafunzi watatu kutoka shule ya upili katika mkoa wa kati wamewekwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja na wengine kadhaa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka kama hayo.

Visa hivyo vimesababisha polisi nchini kuingia katika mtandao wa kijamii kwa kutumia #IFIKIEMASTUDE – kutuma onyo kuhusu hatari itakayowafikia wanafunzi wanaojihusisha na ghasia hizo.

Comments

comments