Kiongozi wa CUF Julius Mtatiro matatani kwa madai ya kumkashifu Rais

Mmoja wa viongozi wa juu wa chama cha upinzani nchini Tanzania CUF Julius Mtatiro anashikiliwa na Polisi nchini Tanzania kwa tuhuma za kudaiwa kutuma ujumbe kupitia ukurasa wake wa facebook ,unaodaiwa kumkashifu Rais Magufuli.

Hatua hii inakuja kufuatia utekelezaji wa sharia mpya ya kimitandao nchini humo,ambayo imekuwa ikipingwa na baadhi ya wanaharakati kwamba inabana uhuru wa kujieleza.Viongozi na wanasheria wa chama hicho wamekuwa wakiendelea na jitihada za kuhakikisha anapata dhamana.

Mtatiro aliandika swali kwenye ukurasa wake wa facebook akiuliza ”Rais kitu gani bwana?” jambo ambalo lilimsababishia kuingia matatani

Kauli yake mtandaoni inadaiwa kuwa imemkashifu Rais Magufuli.

Maafisa wa polisi walienda kufanya ukaguzi nyumbani kwa Mtatiro kuchukua kifaa alichokitumia kuandikia na kuweja ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii.

Julius Mtatiro aliweka ujumbe huo akimuunga mkono kijana mmoja kutoka Mwanza, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, Justine Emmanuel ambaye ndiye awali aliyeuliza swali hilo kwenye ukurasa wake kisha akakamatwa siku tatu zilizopita.

Kuna mipaka kati ya uhuru wa kujieleza na Maadili?

ACT Wazalendo yalalamikia serikali ya Tanzania kuhusu udhibiti wa mitandao

Msemaji wa CUF, Mbarara Maharagambe amesema ”Tunafanya utaratibu wa kushughulikia dhamana yake kwa kuwa dhamana iko wazi”.

Haikuwa wazi swali hilo lilikuwa na maana gani kwa kuwa halikuwa na maelezo zaidi.

Sheria za Tanzania zinaeleza kuwa matamshi au maandiko ya namna hiyo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani

Ikiwa atakutwa na hatia, Mtatiro atakabiliwa na kifungo cha mpaka miezi sita gerezani.

Wanaharakati wa masuala ya haki za binaadamu wamekuwa wakikosoa mamlaka kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza.

Lakini serikali imesema uhuru usio na mipaka unaweza kusababisha uvunjwaji wa amani.

Comments

comments