Ilikuwaje Mtatiro akabadilika na kuwa kada wa CCM?

Maswali mengi yamezuka mara baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) Julius Mtatiro ,kujivua uanachama wake na kuhamia chama tawala cha CCM.

Mtatiro ni mwanasiasa ambaye pia ni mchambuzi wa siasa na amekuwa akiandika makala nyingi kuikosoa serikali lakini sasa amehamia huko ambako amekuwa akikukosoa kwa muda mrefu.

“Nimejiridhisha kwa hitaji la nafsi yangu kujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM” Julius Mtatiro aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari siku ya jumamosi,Agosti 11.

Mkurugenzi wa habari wa chama cha CUF,Abdul Kambaya amesema zaidi ya asilimia 70 ya migogoro ya chama hicho imesababishwa na Mtatiro.

Chama hicho ambacho kimegawanyika katika pande mbili,kuna wale ambao ni wafuasi wa Profesa Ibrahim Lipumba na wale ambao wako chini ya Maalim Seif.

Awali chanzo cha migogoro ya ndani ya chama cha CUF ilidaiwa kuwa ni Profesa Lipumba kutangaza kutengua barua yake ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti aliyoiandika Agosti 2015, wakati wa kuelekea kwenye Uchaguzi mkuu.

Lakini kwa sasa mgawanyiko wa chama hicho umedaiwa kusababishwa na Julius Mtatiro kutokana na tabia zake za kibabe za kutotaka kusikiliza watu wengine.

Inakumbukwa kwamba mwanzoni mwa mwezi Julai,Mtatiro alikamatwa na polisi kutokana na ujumbe alioandika katika mtandao wa kijamii unaomkejeli rais John Magufuli kwa kusema kuwa ‘rais kitu gani?’

Comments

comments