Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM ameachiwa kwa dhamana.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis anayekabiliwa na makosa ya rushwa ameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

 

Sadifa amefikishwa mahakamani leo  baada ya kukosa dhamana Jumatatu Desemba 11,2017 kutokana na upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kiapo kuzuia dhamana kwa madai kuwa angevuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa UVCCM uliofanyika Desemba 10 na 11,2017 mjini Dodoma.

 

Mahakama leo imetupilia mbali pingamizi hilo na kutoa masharti ya dhamana kwamba Sadifa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh1 milioni na wenye vitambulisho vinavyotambuliwa na mamlaka ya maeneo wanakoishi.

 

Sadifa pia ametakiwa kutotoka nje ya mipaka ya nchi bila kibali cha Mahakama. Amekidhi masharti hayo na amechiwa kwa dhamana na kesi itatajwa Januari 18,2018.
Alipofikishwa mahakamani awali, wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo alidai Sadifa anashtakiwa kwa makosa mawili.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa Desemba 9,2017 katika makazi yake kwenye Kata ya Mnada mjini Dodoma akiwa mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.

Sadifa katika shtaka la pili anadaiwa katika eneo hilo na siku hiyohiyo, aliwaahidi kuwalipia usafiri wanachama wa umoja huo kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi huo.

Kutokana na mabishano hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Emmanuel Fovo ameahirisha kesi hadi leo Desemba 19,2017 kutoa nafasi ya mahakama kupitia kiapo kilicholetwa na upande wa mashtaka ili kutoa haki katika maombi ya dhamana ya mshtakiwa. Sadifa alipelekwa rumande.

#Sibukamedia

Comments

comments

Random Posts